NDEJEMBI AMBANA MKANDARASI WA UJENZI SHULE MPYA YA KITANDILILO

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako, Kenneth Haule kuhakikisha mkandarasi aliyepewa kazi ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Kitandililo anaongeza kasi ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

NDEJEMBI AMBANA MKANDARASI WA UJENZI SHULE MPYA YA KITANDILILO
NDEJEMBI AMBANA MKANDARASI WA UJENZI SHULE MPYA YA KITANDILILO

Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kutembelea ujenzi wa shule hiyo mkoani Njombe ambayo ujenzi wake unagharimu kiasi cha Sh.Milioni 683 kupitia mradi wa SEQUIP.

Akizungumza na viongozi na wananchi wa Kata ya Kitandililo, Mhe. Ndejembi ameeleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo ambapo amemtaka mkandarasi kujenga usiku na mchana,  kuongeza idadi ya nguvu kazi ili kutimiza malengo ya serikali ya kukamilisha ujenzi huo ifikapo Oktoba 31 mwaka huu.

“Nimesikitishwa na kasi ya ujenzi wa shule hii, Nchi nzima mwisho wa ujenzi huu ni Oktoba 31 na mimi sitobadilisha muda huo uliopangwa. Nikuagize Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha mnambana Mkandarasi ili aongeze nguvu kazi lakini pia kuongeza muda wa kufanya kazi hadi saa za usiku lengo ni kuhakikisha ujenzi huu unakamilika ndani ya muda uliopangwa.”

” Ninaondoka hapa nikiwa sijaridhishwa na maendeleo ya ujenzi huu, muda wowote nitarejea ili kuona hawa mafundi waliopewa kazi halafu wanabana fedha na hawaweki nguvu ya kutosha na kama hakutakua na mabadiliko hatutosita kuwachukulia hatua watu wenye lengo la kurudisha nyuma jitihada hizi za Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwaletea maendeleo wananchi wa Kata hii,”amesema.

Amesema serikali itahakikisha hakuna mtu yeyote atakayechezea  fedha ama kuchelewesha mradi huo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Charles Msonde amesema atahakikisha anasimamia maelekezo hayo ili  ujenzi wa shule hiyo ukamilike ndani ya muda uliopangwa.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Ndejembi ametembelea Shule ya Msingi Azimio ambayo imefanyiwa maboresho kupitia mradi wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji kwa Shule za Awali na Msingi (BOOST) na kueleza  kuridhishwa na ujenzi wa shule hiyo.

Kwamaelezo zaidi tembelea; https://www.tamisemi.go.tz/new

Leave a Comment