Mfumo wa maombi ya ajira Tamisemi; Nchi yetu ilipata uhuru tarehe 09.12.1961 ambapo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alimteua Mhe.Job Lusinde Waziri wa Kwanza wa Wizara ya Serikali za Mitaa, akifuatiwa na Mawaziri 22 wakiwemo wanawake 3. Kwa sasa Wizara hiyo inaongozwa na Mhe Mohamed Mchengerwa
Tangu mwaka 1961 hadi sasa Ofisi ya Rais –TAMISEMI imekuwa ni Wizara inayojitegemea, Wizara chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kwenye Ofisi ya Rais kama ilivyo sasa. Uamuzi wa wapi inawekwa umekuwa ukifanyika ili kuimarisha utendaji wa Ofisi hii.
Ofisi ya Rais TAMISEMI ni Wizara pekee ambayo Makao Makuu yake yalianzia Jijini Dodoma tangu mwanzoni mwa miaka ya sabini tangu Serikali ilipotangaza Makao Makuu ya Serikali kuwa ni Dodoma na kwa Dar es salaam kumekuwa na Ofisi ndogo. Uwepo wa Makao Makuu Dodoma ulikua na lengo la kutoa fursa sawa kwa wadau wake wakuu hususan Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kufika Dodoma kwa urahisi wanapofuata huduma mbalimbali.
Madhumuni ya kuwepo kwa Serikali za Mitaa ni kupeleka Madaraka kwa Wananchi ambapo chimbuko lake ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika Sura ya 8, Ibara ya 145 na 146. Upelekeaji wa madaraka kwa wananchi unapitia katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na ndiyo maana Serikali za Mitaa na ushirikishwaji wa Wananchi katika mchakato wa maendeleo vimetambuliwa katika Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakati Nchi yetu inapata uhuru wake kulikuwa na majimbo kumi ya Utawala ambayo yaliritihiwa toka utawala wa kikoloni wa Kiingereza mwaka 1966. Rais wa kwanza Hayati Julius Kambarage Nyerere kwa Mamlaka aliyopewa aliunda Mikoa 15 na kuondoa utaratibu wa mgawanyo wa nchi katika Majimbo. Hadi Sasa Nchi yetu ina Mikoa 26, Wilaya 139, Halmashauri 184, Tarafa 570, Kata 3,956, Vijiji 12,319, Vitongoji 64,384 pamoja na Mitaa 4,263. Baada ya uhuru Halmashauri zilikuwa jumla 45 na hadi kufikia mwaka 2009 zilikuwa Halmashauri 129 na zimeendelea kuongezeka hadi kufikia 184 mwaka 2021.
Wakati wa Uhuru hakukuwa na Halmashauri za Majiji na sasa kuna Halmashauri za Majiji 6, kulikuwa na Halmashauri ya Manispaa moja ya Dares Salaam na sasa kuna Halmashauri za Manispaa 20, Halmashauri za Miji zilikuwa 9 na sasa Halmashauri za Miji ni 21 na Halmashauri za Wilaya zilikuwa 10 na sasa zipo Halmashauri za Wilaya 137.
Serikali iliendelea na mfumo wa Serikali za Mitaa uliorithiwa kutoka kwa Wakoloni na kuutumia kama nyenzo za kuleta maendeleo kwa misingi ya Kidemokrasia. Kutokana na changamoto mbalimbali zilizoukabili utendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa baada ya uhuru mwanzoni mwa miaka ya sabini, Serikali ilifuta Mamlaka hizi na kuanzisha mfumo wa Madaraka Mikoani.
Mfumo huu ulizifanya Serikali za Mitaa kuitegemea Serikali Kuu kwa kila jambo kutokana na wananchi kutoshiriki katika maamuzi na pia katika shughuli za maendeleo, uchumi wa nchi ulididimia na viwango vya maisha kushuka. Kutokana na hali hii, Serikali za Mitaa kwa upande wa Mamlaka za Miji zilirejeshwa tena mwaka 1978 na mwaka 1984 Serikali za Mitaa zilirejeshwa upande wa Mamlaka za Wilaya pia zilirejeshwa.
Kwa lengo la kuziimarisha Serikali za Mitaa na kuziwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali. Mojawapo ya hatua hizi ni kuanzishwa kwa Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa ulioanzishwa mwaka 1998 ambao ulilenga katika kupeleka madaraka kwa Wananchi (D by D).
Katika kipindi hicho cha Maboresho, Serikali ilitoa Tamko la Kisera la Ugatuaji wa Madaraka- Policy Paper on Local Government Reform Programme on Decentralization by Devolution (D-by-D) kama njia muafaka ya kufikisha na kuharakisha maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi na kuinua utoaji wa huduma kwa wananchi. Uamuzi huu wa kisera umelenga kuondokana na mapungufu yaliyokuwepo katika Mifumo ya awali na kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizokuwepo.
Dhana hii ya D by D imejengwa kwa misingi ya kutoka kwenye mfumo wa Madaraka ya Serikali Kuu kuwa na maamuzi yote na Serikali za Mitaa kuwa Mtekelezaji tu (yaani Mwagizaji na Mtekelezaji) kwenda katika mfumo wa Serikali za Mitaa wenye Mamlaka ya Kisheria ya kuamua mambo katika eneo lao na kuyatekeleza. Hivyo, kuwa na mfumo wa mahusiano ya majadiliano katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo. Dhana hii inalenga kupeleka madaraka zaidi kwa wananchi.
Maelekezo.
- Tafadhali chagua aina ya maombi ya ajira kama ni AFYA au ELIMU
- Kama ni muombaji mpya bofya kiunganishi cha juu kulia “Jisajili” kuanza kuomba
- Ingiza namba ya NIDA au barua pepe kama jina la mtumiaji na uingize nywila yako kuingia ndani ya mfumo.
- Baada ya kufanikiwa kuingia ndani, tafadhali kamilisha maombi yako kabla ya tarehe ya mwisho
- Maombi yasiyokamilika hayatafanyiwa kazi
- Hakikisha kabla ya kutuma maombi umesoma na kuelewa vizuri tangazo lilotolewa
- Hakikisha vyeti ulivyo ambatanisha vinasomeka vizuri
- Kuwasilisha taarifa za kughushi zitapelekea kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi yako
- Bofya hapa ili ujisajili kwa ajili ya kutuma maombi
Kwa Msaada
Tafadhali piga simu huduma kwa mteja : 026-2160210 au 0735-160210.